Monday, October 28, 2013

BBC SWAHILI:Polisi wavamia kituo cha redio SomaliaPolisi nchini Somalia walivamia makao makuu ya kituo cha redio cha Shabelle, na kukilazimisha kufunga matangazo yake mnamo siku Jumamosi.
Maafisa wakuu wanasema kuwa wanadhibiti jengo hilo ambalo lilikuwa linamilikiwa na serikali miaka ya nyuma.
Kituo hicho kinasifika kwa kukosoa sana maafisa wakuu wa serikali.
Hatua ya kudhibiti jengo la kituo hicho, ni ya hivi karibuni katika mfululizo wa mashambulizi dhidi ya waandishi huru wa habari ambayo yamekuwa yakifanywa na serikali sawa na kundi la kigaidi la al-Shabaab.
Kituo hicho hata hivyo kiliwahi kutakiwa kuondoka katika jumba hilo.
Maafisa wa usalama wanasema kuwa notisi ya siku tano waliyotoa kwa wakuu wa kituo hicho kuwataka kuondoka katika jumba hilo imefika mwisho lakini wakuu wa kituo hicho wanasema kuwa wanakodisha jumba hilo kihalali kwa mujibu wa mkataba waliokuwa nao na serikali iliyotangulia.
Serikali ya Somalia iko katika harakati ya kumiliki majengo na taasisi zilizokuwa zinamilikiwa na serikali ya awali.
Wanaharakati wanasema kwua hatua hii itahatarisha maisha ya waandishi wa habari, wengi wanaoishi katika jengo hilo.
Radio Shabelle iliripoti kwenye mtandao wake kuwa polisi waliingia katika jengo hilo kwa lazima na hata kuwachapa baadhi ya waandishi waliokuwa kazini.
Walioshuhudia tukio hilo walifahamisha shirika la habari la AFP kuwa wafanyakazi wa rediao hiyo walionekana wakiwekwa ndani ya lori za polisi kwa nguvu.
Hata hivyo polisi walikana kuwa operesheni yao ilikuwa inalenga shughuli za kituo hicho kwani kinasifika sana kwa kuwa wakosoaji wakuu wa serikali.
Waziri wa mambo ya ndani anasema kuwa jengo hilo lilikuwa ofisi za shirika la ndege la Somalia na kwa hivyo basi linapaswa kurejeshwa kwa serikali.
Aidha wakuu wa kituo hicho wanasema kuwa walikuwa wanatumia jengo hilo lililokaribu na uwanja wa ndege kihalali baada ya makubaliano kati yao na serikali ya awali.
Waandishi wa habari nchini Somalia ni baadhi ya wanaokabiliwa na tisho kubwa la usama dhidi ya maisha yao kama waandishi, hii ni kwa mujibu wa shirika la waandishi wasio na mipaka.
Waandishi habari 18 waliuawa nchini Somalia mwaka 2012 huku shirika hilo likisema kuwa waandishi 10 wa Redio Shabelle wameuawa tangu mwaka 2007.

0 comments: