Saturday, September 01, 2012

BI KIDUDE TUMUOMBEENI, HALI YAKE MBAYA HINDU MANDAL

Na Princess Asia
HALI ya afya ya msanii mkongwe nchini, Fatuma Bint Baraka, maarufu Bi Kidude ni mbaya na akiwa amehamishwa kutoka Zanzibar hadi katika hospitali ya Hindu Mandali Dar es Salaam na jana watu walikuwa wanazuiwa kwenda kumuona.
Bi Kidude alianza kusumbuliwa na maradhi mwezi uliopita, lakini baadaye akapata ahueni na kufanya mahojiano hadi na vyombo vya habari, lakini ghafla mambo yamebadilika tena na amerudi hospitali.
Bi Kidude ni gwiji wa muziki katika Bara la Afrika, katika fani ya muziki wa mwambao ambao hujulikana kwa jina la Taarabu. Muziki huu ambao ni mchanganyiko wa muziki toka nchi za Kiarabu na vionjo vya muziki wa Kiafrika umekita sana katika mwambao wa Afrika Mashariki yaani Zanzibar, Mombasa, Lamu na kwingineko.
Fatuma binti Baraka au Bi Kidude, alizaliwa katika kijiji cha Mfagimarigo Zanzibar katika familia ya watoto saba (7). Baba yake Mzee Baraka alikuwa ni mfanyabiashara wa nazi, zao ambalo ni la kutumainiwa sana Zanzibar.
Bi Kidude anasema hafahamu tarehe halisi aliyozaliwa, isipokuwa anachojua ni kwamba alizaliwa wakati rupia ikitumika kama fedha, na vilevile ana hakika ni kabla ya Vita Kuu ya Kwanza ya Ulaya.
Wataalamu wa mahesabu baada ya kupata taarifa hizo wakampigia mahesabu na kumkabidhi miaka yake kwamba ni zaidi ya miaka 90.
Bi Kidude anasema uimbaji aliuanza tangu alipokuwa na umri wa miaka 10 na alijifunza kutoka kwa msanii mkongwe na aliyetamba sana enzi hizo Sitti Binti Saad. Anasema wageni wengi kutoka sehemu mbalimbali walikuwa wakifika Zanzibar kuja kumwona Sitti, na kwa vile Bi Kidude na Sitti walikuwa wako karibu basi yeye alikuwa akiwapeleka wageni wale nyumbani kwa Bi Sitti, wakifika huko wageni walikuwa wakiingia ndani na yeye kubakia nje, kule ndani Bi Sitti alikuwa akiwaimbia wale wageni, na yeye huku nje alikuwa akimsikiliza kwa makini na kumfuatiza jinsi alivyokuwa akiimba. Aliendelea hivyo hadi akawa mahiri sana katika uimbaji.
Alipokuwa na miaka 13, kwa mara ya kwanza alitoroka nyumbani kwao Zanzibar na kukimbilia Tanzania Bara, baada ya kulazimishwa kuolewa. Lakini alipokuwa kigoli wa kutosha kuolewa aliolewa ingawa ndoa hiyo nayo haikudumu kutokana na manyanyaso aliyokuwa akiyapata, hivyo aliamua kukimbilia kaskazini mwa Misri ikiwa ni katika miaka ya 1930, huko aling'ara sana katika fani yake ya uimbaji na uchezaji ngoma. Lakini ilipofika miaka ya 1940 aliamua kurudi nyumbani Zanzibar ambako aliendelea na shughuli zake uimbaji.
Bi Kidude hategemei kazi moja tu ya kuimba, kwani pia ni mfanyabiashara ya 'wanja' na 'hina' ambavyo anavitengeneza yeye mwenyewe, pia ni mtaalamu wa matibabu kwa dawa za mitishamba na zaidi ya hayo ni mwalimu mzuri sana wa 'Unyago' na ameanzisha chuo chake mwenyewe na anasema katika wanafunzi wake wote hakuna aliyepata talaka kutoka kwa mumewe.
Watu wanasema 'Utu uzima dawa' Bi Kidude ana upeo mkubwa sana wa akili kwani pamoja na kukulia katika mazingira yaliyogubikwa na tamaduni za kiarabu ambapo mwanamke anatakiwa wakati wote akiwa hadharani ajifunike, Bi Kidude aliliona hili katika upeo mwingine kwamba ni sheria tu ya kitamaduni toka Uarabuni, hivyo aliamua kuvunja sheria hiyo na kuondoa hijabu mwilini mwake, na sasa hivi anavaa kama Mtanzania na si kama Mwarabu. Lakini hakubakia hapo alivunja na miiko mingine zaidi ya kutokunywa na kuvuta, kwani Bi Kidude anakunywa pombe na kuvuta sigara jambo ambalo si kawaida kwa wanawake Zanzibar.
Bi Kidude amekwisha tembelea nchi nyingi sana ikiwa ni pamoja na Oman, Ufaransa, Hispania, Ufini, Ujerumani na Uingereza.
Amekwisha pata tuzo mbalimbali ikiwa ni pamoja na ile ya Tamasha la Filamu la Nchi za Jahazi (ZIFF) mwaka 1999 tuzo ni ya maisha. Pia mwaka jana tuzo ya WOMAX ilienda kwake.
Nyimbo alizowahi kuimba ni pamoja na Muhogo wa jang'ombe, na anaimba kwa Kiswahili na Kiarabu. Hakuwahi kupata elimu nyingine zaidi ya Kurani. SWAHILIINFO inaungana na Watanzania wote kumtakia kila la heri Bi Kidude, apone na kurejea nyumbani.

0 comments: