Saturday, May 10, 2014

Rais Kikwete afanya mazunguzo na Samatta na Ulimwengu nchini Congo..

 

Na Mahmoud Zubeiry, Dar es Salaam
RAIS wa Jamhuri ya Muungano Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete leo amewatembelea washambuliaji wawili Watanzania wanaocheza TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Mbwana Ally Samatta na Thomas Emannuel Ulimwengu.
 
Tovuti ya TPM imeandika kwamba Rais Kikwete aliwatembelea wachezaji hao leo mjini Kinshasa ambako wapo na timu yao kwa ajili ya mchezo wa Ligi Kuu ya DRC dhidi ya mahasimu wao katika mbio za ubingwa AS Vita.

Rais Kikwete aliye ziarani DRC, alikuwa ameambatana na maofisa wawili wa Ubalozi wa Tanzania majira ya Saa 6:15  mchana alipokutana na wachezaji hao pamoja na Mwenyekiti  wa klabu yao, Moses Katumbi.
Rais Kikwete yupo Kinshasa tangu jana usiku kwa ziara maalum ya Saa 24 juu ya ushirikiano wa DRC na Tanzania, ambako alikutana na rais mwenzake wa huko, Joseph Kabila.
Kikwete alitumia robo saa kuzungumza na akina Samatta katika hoteli ya Congo River, ambako wameweka kambi kwa ajili ya mechi ya kukata na shoka kesho.

Rais Kikwete aliwakumbusha Samatta na Ulimwengu kwamba, Watanzania wanajivunia kuwaona wakiwa na jezi za TPM na kwamba wao ni tegemeo la timu ya taifa, Taifa Stars kwa sasa.

0 comments: